Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kobler alaani mashambulizi ya kigaidi Libya

Kobler alaani mashambulizi ya kigaidi Libya

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Martin Kobler amelaani vikali mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea leo dhidi ya kituo cha mafunzo ya usalama mjini Zliten.

Bwana Kobler ambaye pia ni mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNSMIL ameeleza kushtushwa sana na shambulio hilo. Ametuma salamu zake za rambirambi kwa familia za wahanga na kuwatakia nafuu waliojeruhiwa.

Ameongeza kwamba tukio hilo linalochukiza ni ishara ya umuhimu wa kuunda serikali ya mwafaka wa kitaifa na kufufua vikosi vya usalama nchini humo.

Taarifa iliyotolewa leo imeeleza kwamba Umoja wa Mataifa utashirikiana na mamlaka za afya za eneo hilo ili kufikisha vifaa tiba.

Bwana Kobler amewasihi Walibya kushikamana ili kupambana na ugaidi, akisema Libya haiwezi kuendelea kugawanyika wakati wa tishio hilo la kigaidi.