Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

China kufunga machimbo ya makaa ya mawe kudhibiti uchafuzi wa hewa

China kufunga machimbo ya makaa ya mawe kudhibiti uchafuzi wa hewa

Mamlaka ya taifa ya nishati nchini China, NEA haitoidhinisha machimbo mapya ya makaa ya mawe nchini humo ndani ya kipindi cha miaka mitatu ijayo, ikiwa ni  hatua za kudhibiti utoaji wa gesi chafuzi.

Katika taarifa iliyotolewa leo, mamlaka hiyo imesema pamoja na  hatua hizo,  machimbo mengine zaidi ya 1,000 yanayofanya kazi sasa yatafungwa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu na hivyo kupunguza uzalishaji wa makaa ya mawe kwa asilimia 70.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa mambo, hii ni mara ya kwanza kwa China kupiga marufuku uanzishwaji wa machimbo mapya ya makaa ya maweI na hatua hiyo imechochewa na kushuka kwa mahitaji ya makaa hayo halikadhalika ongezeko la hofu ya wananchi juu ya kiwango cha uchafuzi.

Mwezi Disemba, mji kuu wa China, Beijing ulitangaza mara mbili tahadhari ya juu zaidi ya moshi mzito kwenye anga lake na kusababisha shule kufungwa na wakazi kutakiwa kusalia majumbani.

Tafiti zinaonyesha kuwa nchini China, uchafuzi wa hewa unasababisha vifo vya watu wapatao Milioni Moja nukta Sita kila mwaka.