Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Naondoka Mali nikiwa na matumaini; Hamdi

Naondoka Mali nikiwa na matumaini; Hamdi

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, Mongi Hamdi amesema anaondoka Mali na moyo wa amani na uaminifu kuhusu mchakato wa amani.

Amesema hayo kwenye ujumbe wake wa mwisho akihitimisha muda wake kama mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMA, akimshukuru Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita, wawakilishi wa serikali na jamii wa Mali kwa ushirikiano wao na MINUSMA katika kujenga amani ya kudumu nchini humo.

Bwana Hamdi amesema amejifunza mengi katika muda wake nchini Mali, akipongeza raia kwa upendo wao kwa nchi yao licha ya changamoto zilizoikumba ikiwemo mashambulizi ya kigaidi ambayo amesema hayakuweza kudhoofisha umoja wa nchi hiyo.

Hatimaye Bwana Hamdi ameisihi jamii ya kimataifa kusaidia Mali katika kupambana na ugaidi.

Bwana Mahamat Saleh Annadif ndiye anatarajiwa kuchukua nafasi ya Hamdi huko Mali.