Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zeid aitaka Thailand kuchunguza kikamilifu kutoweka kwa watu

Zeid aitaka Thailand kuchunguza kikamilifu kutoweka kwa watu

Kamishina mkuu wa haki za binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein Jumatano ameitaka serikali ya Thailand kuchukua hatua na kuchunguza kikamilifu wapi walipo watu takribani 82 walioorodheshwa kama wametoweka akiwemo mwanasheria anayeheshimika sana nchini humo Somchai Neelapaijit, aliyetoweka yapata miaka 12 iliyopita.

Zeid pia ameitaka serikali ya Thai kujumuisha katika sharia zake kitendo cha kutowesha watu kama ni kosa la jinai kwa mujibu wa viwango vya kimataifa. Ameongeza kuwa familia za watu wote hao waliotoweka zina haki ya kujua ukweli kuhusu kutoweka kwao pamoja na hatua zozote ziloizochukuliwa na matokeo ya uchunguzi.

Tarehe 29 Desemba 2015 mahakama kuu ya Thailand ilizingatia uamuzi wa mahakama ya rufaa wa kuwaachia maafisa wa polisi watano watuhumiwa kuhusika katika utekaji na upotevu wa Somchai, mwanasheria Muislam ambaye alipotea Machi 12, 2004 wakati alipokuwa akiwatetea watu waliokamatwa chini ya sheria ya kijeshi katika eneo la kusini mwa nchi hiyo. Watuhumiwa walikuwa wanaishutumu serikali kuwatesa wakiwa kizuizini.

Mashahidi wamearifu kumuona Somchai akilazimishwa kupanda kwenye gari usiku aliodaiwa kutoweka. Mawaziri wakuu wawili wanchi hiyo walitoa wito wa kufanyika uchunguzi ili kutatua kitendawili cha kutoweka kwa bwana Somchai bila mafanikio yoyote.