Skip to main content

Waliofurushwa makwao Iraq wahaha kwa mapigano zaidi na baridi

Waliofurushwa makwao Iraq wahaha kwa mapigano zaidi na baridi

Watu wapatao 400,000 nchini Iraq hawana makazi ya kutosha huku wengine 780,000 wakiishi bila bidhaa muhimu za nyumbani na za kuendeleza ubora wa maisha yao wakati huu wa msimu wa baridi kali, limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Masuala ya Kibinadamu, OCHA.

Kwa mujibu wa OCHA, serikali ya Iraq na wadau wa kitaifa na kimataifa wanaoa usaidizi wa vifaa vya kupasha moto mahema, nguo za joto, fedha, mafuta na vifaa vingine vya kuboresha hali ya maisha.

Miongoni mwa wadau wa kimataifa ni Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM.

Wakati huo huo, OCHA imesema kambi mpya iliyofunguliwa ya Al Qaser sasa inahifadhi familia 135 za wakimbizi wa ndani kufuatia mapigano yanayoendelea katika maeneo ya Ramadi katika mkoa wa Anbar nchini Iraq, huku familia 6,000 zilizofurushwa makwao katika mapigano Ramadi mapema mwaka uliopita bado zinahifadhiwa katika mji wa utalii wa Habbaniya.