Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 9 wafariki dunia katika tetemeko la ardhi India na Bangladesh

Watu 9 wafariki dunia katika tetemeko la ardhi India na Bangladesh

Watu wapatao tisa wameripotiwa kufariki dunia leo Jumatatu Januari 4, kufuatia tetemeko la ardhi lililolikumba jimbo la Manipur nchini India, na kuathiri pia nchi jirani za Bangladesh na Myanmar, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu, OCHA.

Miongoni mwa walioripotiwa kufariki dunia katika tetemeko hilo lenye ukubwa wa 6.7 kwenye kipimo cha richa, ni watu wanane nchini India na mtu mmoja nchini Bangladesh, huku watu zaidi ya 100 wakiripotiwa kujeruhiwa, hususan kwa maporomoko ya nyumba karibu mji mkuu wa jimbo la Manipur, Imphal.

Ukubwa wa hasara kwa majengo na miundombinu mingine katika maeneo yaliyoathiriwa bado haujadhihirika. Hadi sasa, hakuna ripoti zozote kuhusu madhara ya tetemeko hilo katika majimbo ya Chin na Sagaing nchini Myanmar, ambako tetemeko hilo lilihisiwa.

Shirika la OCHA limesema serikali na wadau wa kibinadamu wanafuatilia hali iwapo kutakuwa na madhara zaidi, na kwamba hadi sasa mamlaka za India hazitarajiwi kuomba msaada wa kimataifa.