Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ethiopia yakumbwa na ukame mkali, WFP yatoa wito kwa ufadhili

Ethiopia yakumbwa na ukame mkali, WFP yatoa wito kwa ufadhili

Nchini Ethiopia, mahitaji ya kibinadamu yameongezeka mara tatu tangu mwanzo wa mwaka 2015 kutokana na ukame mkali unaokumba baadhi ya maeneo ya nchi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula WFP limesema El-Nino ambayo mwaka huu imekuwa mbaya zaidi imehatarisha zaidi hali hiyo na kusababisha mazao kuharibika, na mifugo kufa kwa wingi, huku utapiamlo wa kupindukia ukiathiri nusu ya wilaya za Ethiopia.

Aidha taarifa ya WFP imeeleza kwamba shirika hilo linatarajia kusaidia serikali kufikia watu milioni 7.6 mwaka 2016 miongoni mwa milioni 10 wanaohitaji msaada. Hata hivyo WFP imesema ni asilimia 5 tu ya mahitaji ambayo yamefadhiliwa.

Licha ya jitihada kubwa za serikali katika kudhibiti mzozo huo, WFP imesema usaidizi wa kimataifa unahitajika.