Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kobler ataka mwaka 2016 usiwe mwaka wa kurudi nyuma Libya

Kobler ataka mwaka 2016 usiwe mwaka wa kurudi nyuma Libya

Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Martin Kobler, amezuru Libya tarehe mosi Januari kwa mara ya kwanza baada ya kuteuliwa, akisema mwaka 2016 ni mwaka wa kutekeleza makubaliano ya kisiasa na kujenga amani ya kudumu nchini humo.

Akihojiwa na redio ya Umoja wa Mataifa, Bwana Kobler amesema makubaliano ya kisiasa yaliyosainiwa tarehe 17 Disemba mwaka 2105 mijini Skhirat yamekuwa yakishirikisha wawakilishi wa pande zote za mzozo na wa jamii, akiongeza kwamba hataki yazungumziwe upya, bali yaanze kutekelezwa kwa manufaa ya walibya.

Ameeleza alichoshuhudia alipotembelea Libya.

(Sauti ya Bwana Kobler)

“Na wote wanataka kuwa na usalama. Bei za bidhaa muhimu zinapanda. Dawa katika hospitali zinazidi kuwa haba. Akiba ya Benki kuu inadidimia. Hali haiwezi kuendelea hivi. Kwa hiyo, watu wa Libya wanastahili hali bora zaidi, na ninahisi kuwa asilimia 95, la hata asilimia 99 ya watu wa kawaida wanaunga mkono makubaliano haya”

Bwana Kobler ameziomba pande zote kuwajibika na kuchukua fursa ya kuunda serikali jumuishi, akisema ataendelea kujitahidi kushawishi washikadau kuunga mkono mchakato huo.