Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Ki-moon alaani mauaji ya Sheikh Al-Nimr nchini Saudia

Ban Ki-moon alaani mauaji ya Sheikh Al-Nimr nchini Saudia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, ameeleza kushtushwa sana na mauaji ya watu 47 nchini Saudi Arabia, akiwemo Sheikh Nimr Baqir Al-Nimr, kama ilivyotangazwa na Waziri wa Mambo ya Ndani Jumamosi hii.

Bwana Ban amesema hayo kwenye taarifa iliyotolewa na msemaji wake, akiongeza kwamba alikuwa amezungumzia kesi ya Sheikh Al-Nimr mara kadhaa na uongozi wa Saudia.

Sheikh An-Nimr na wafungwa wengine waliouawa tarehe pili Januari walihukumiwa kifo baada ya kesi iliyozua mashaka kuhusu usawa wake.

Aidha Katibu Mkuu amekariri msimamo wake wa kupinga adhabu ya kifo akiiomba Saudia kusitisha kutekeleza adhabu zote za kifo zilizohukumiwa nchini humo.

Hatimaye ametoa wito kwa utulivu akiwaomba viongozi wa ukanda wa Mashariki ya Kati kujizuia kuchochea mivutano ya kidini kufuatia kifo hicho, akilaani pia ghasia katika maandamano dhidi ya ubalozi wa Saudia nchini Iran.