Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICTR yahitimisha kazi leo, Baraza la Usalama latoa pongezi

ICTR yahitimisha kazi leo, Baraza la Usalama latoa pongezi

Wanachama wa Baraza la Usalama wamepongeza kazi zilizofanyika na mahakama ya kimataifa kuhusu mauaji ya kimbari Rwanda ICTR ambayo inahitimisha kazi zake leo.

Kwenye taarifa yake Baraza la Usalama limemulika mchango wa ICTR katika mchakato wa maridhiano nchini Rwanda, pamoja na kurejesha amani na usalama nchini humo na kupambana na ukwepaji sheria.

Aidha limesema kwamba kuundwa kwa mahakama hiyo kulisaidia kukuza sheria ya kimataifa kuhusu mauaji ya kimbari duniani kote.

Halikadhalika, wanachama wa Baraza hilo wameziomba nchi kushirikiana na serikali ya Rwanda pamoja na Mfumo wa kushughulikia kesi zilizobaki, ulioundwa ili kukamata na kufuatilia kesi za watu nane walioshtakiwa na ICTR na ambao wamekimbia sheria.