Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ampa heko rais moya wa Burkina Faso na kuupongeza upinzani

Ban ampa heko rais moya wa Burkina Faso na kuupongeza upinzani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, ametuma risala za pongezi kwa Bwana Roch Marc Christian Kaboré, kufuatia kuapishwa kwake leo kuwa rais wa  Burkina Faso.

Ban amemtakia rais huyo mpya ufanisi katika kutimiza majukumu yake ya kuiongoza nchi yake kuelekea ustawi, utawala wa demokrasia, ulinzi wa haki za binadamu, na maendeleo kiuchumi.

Katibu Mkuu ameutaja wakati huu kuwa wa kihistoria kwa taifa la Burkina Faso, na kuwapongeza watu wake na viongozi wa kisiasa kwa kuonyesha mfano mzuri wa kufanya uchaguzi huo wa Novemba 29 kwa amani na uwajibikaji.

Amewasifu pia viongozi wa upinzani kwa kumpa pongezi rais mteule mara tu baada ya matokeo kutangazwa.

Aidha, amempongeza Bwana Michel Kafando na mamlaka za mpito kwa juhudi zilizopelekea kufanyika uchaguzi huo haraka, na kwa kukabiliana na changamoto zilizoibuka wakati wa mpito, kufuatia kutimuliwa kwa rais wa zamani, Blaise Compaoré mnamo Oktoba mwaka 2014.