Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wahimiza serikali zichukue hatua kupunguza madhara ya majanga ya hali ya hewa

UM wahimiza serikali zichukue hatua kupunguza madhara ya majanga ya hali ya hewa

Kufuatia vimbunga vilivyoishambulia Marekani wakati wa Krismasi, kunyesha kwa barafu Mexico na mafuriko Amerika ya Kusini na Uingereza, Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza madhara ya majanga, Margareta Wahlström, ametoa wito kwa serikali zichukuwe hatua za tahadhari ili kupunguza hasara za kwa binadamu na kiuchumi zinazotokana na majanga ya hali ya hewa.

Bi Wahlström amesema mnamo Mwezi Machi mwaka huu, viongozi wa dunia walikutana mjini Sendai, Japan, na kukubaliana kuhusu mkakati mpya wa kimataifa kuhusu kupunguza madhara ya majanga ili kuulinda ulimwengu vyema zaidi kutokana na majanga yanayoongezeka, akiongeza kuwa mkakati huo una malengo saba yatakayozisaidia nchi na jamii kudhibiti hatari zitokanazo na tabianchi.

Bi Wahlström amesema mamilioni ya watu wamo hatarini zaidi kutokana na ukuaji wa miji, na kuongeza kuwa hatua za kuzuia ni muhimu katika kuwalinda watu wengi hata zaidi kutokana na madhara ya majanga. Amezitaja baadhi ya hatua hizo kama kuboresha mifumo ya tahadhari za awali ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kufanyia marekebisho kanuni za ujenzi ili kuboresha uthabiti wa miundombinu muhimu kama vile shule, hospitali, barabara, na kuwekeza katika vizuizi vya mafuriko.

Zaidi ya watu 20 walifariki dunia katika mwishoni mwa wiki iliyopita kutokana na vimbunga katika majimbo ya New Mexico, Texas, Oklahoma, Missouri na Illinois nchini Marekani na kuharibu mamia ya majengo na nyumba.