Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO yapata Kamanda mpya: ni Luteni Jenerali Mgwebi wa Afrika Kusini

MONUSCO yapata Kamanda mpya: ni Luteni Jenerali Mgwebi wa Afrika Kusini

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametangaza leo kwamba amemteua Luteni Jenerali Derick Mbuyiselo Mgwebi wa Afrika Kusini kuwa Kamanda wa vikosi vya Umoja wa Mataifa vya kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), MONUSCO.

Luteni Jenerali Mgwebi anamrithi Luteni Jenerali Carlos Alberto dos Santos Cruz wa Brazil, ambaye amekamilisha muda wake wa kuhudumu mnamo Disemba 2 mwaka 2015.

Ban amemshukuru Jenerali Cruz kwa kazi na mchango wake kwa MONUSCO katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Luteni Jenerali Mgwebi, ambaye sasa ni Mkuu wa Operesheni za pamoja za vikosi vya ulinzi vya Afrika Kusini, ana uzoefu wa zaidi ya miaka 35 katika jeshi kitaifa na kimataifa. ALiwahi kuhudumu kama Kamanda wa vikosi vya Umoja wa Mataifa Burundi (ONUB) kati ya mwaka 2004 na 2006.