Kobler akaribisha azimio la Baraza la Usalama kuhusu Libya
Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, UNSMIL, Martin Kobler, amekaribisha azimio lililopitishwa leo kwa kauli moja na Baraza la Usalama la Umoja huo leo mchana, likikaribisha makubaliano ya kisiasa ya Libya yaliyosainiwa mnamo Disemba 17, 2015, kama hatua muhimu kwenye barabara ya kuelekea amani, usalama na maendeleo.
Amesema azimio hilo la leo ni kauli dhahiri na thabiti ya uungaji mkono makubaliano ya kisiasa ya Libya na taasisi zinazotokana nayo. Amesema jamii ya kimataifa imeungana kwa ajili ya amani Libya.
Mbali na kukaribisha makubaliano hayo, azimio la Baraza la Usalama limekaribisha kuundwa kwa Baraza la Urais na kutoa wito baraza hilo lijikite hima katika kuunda serikali ya umoja wa kitaifa katika kipindi cha siku 30 zilizotajwa katika makubaliano hayo ya kisiasa.
Bwana Kobler amesema kuwa pande za kisiasa nchini Libyan ni lazima ziongeze juhudi zao za kutekeleza haraka makubaliano hayo yaliyosainiwa mjini Skhirat, Morocco, na kwamba ujumbe wa UNSMIL unatazamia kushirikiana nao katika kuunga mkono serikali itakayoundwa ya umoja wa kitaifa.