Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lataka maazimio yake kuhusu Yemen yatekelezwe

Baraza la Usalama lataka maazimio yake kuhusu Yemen yatekelezwe

Wajumbe wa Baraza la Usalama wamekariri wito wao wa kutaka utekelezaji kamili wa maazimio ya baraza hilo kuhusu haja ya kuwepo mchakato wa mpito nchini Yemen, ambao ni wa amani, utaratibu na jumuishi, na kuzitaka pande zote Yemen kurejelea hima mashauriano yanayoendeshwa na Umoja wa Mataifa, kulingana na azimio lake nambari 2216 la mwaka 2015.

Wajumbe hao wa Baraza la Usalama wamezipongeza pande husika Yemen na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa kukamilisha awamu ya mchakato wa mazungumzo ya amani hivi karibuni, ambayo yameweka msingi wa awamu zitakazofuata za mchakato wa amani.

Wamekaribisha makubaliano ya pande kinzani kusitisha uhasama, huku wakielezea kusikitishwa na idadi kubwa ya ukiukwaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano uliofanyika wakati wa mazungumzo.

Wamesisitiza kuwa usitishaji mapigano na kuheshimu maazimio husika ya Baraza la Usalama kutaweza kuleta amani ya kudumu.