Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali yaendelea kuwa tete Yemen:Zeid

Hali yaendelea kuwa tete Yemen:Zeid

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa na mjadala maalum kuhusu hali ya usalama na kibinadamu nchini Yemen, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Zeid Ra'ad Al Hussein akionya kwamba hali ikiendelea kuzorota nchini humo, Yemen iko hatarini kusambaratika na kugeuka hifadhi kwa wagaidi na hivyo kuhatarisha amani ya kikanda.

Akihutubia mkutano huo mjini New York, Marekani, Kamishna Zeid amesisitiza kwamba asilimia 80 ya raia wa Yemen wanategemea misaada ya kibinadamu. Amelaani mashambulizi ya makombora yanayoathiri maeneo yanayokaliwa na raia na majengo ya umma kama vile hospitali na shule akisema kwa kiasi kikubwa mashambulizi hayo yanatekelezwa na muungano unaoendeshwa na Saudia.

Kwa upande wake Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen, Ismael Ould Cheikh Ahmed ameeleza kwamba hali ya usalama Yemeninawapa waasi wa kigaidi wa Al-Qaeda nafasi ya kuenea kusini mwa nchi.

Tangu mwanzo wa mgogoro nchini Yemen, watu zaidi ya 2,700 wameuawa, wakiwemo watoto 600. Mazungumzo ya amani yalianza wiki iliyopita mjini Geneva Uswisi, lakini yamehairishwa hadi mwezi Januari baada ya kuvunjika kwa usitishwaji mapigano.