Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO yahamasisha waandishi wa habari kuhusu uchaguzi DRC

MONUSCO yahamasisha waandishi wa habari kuhusu uchaguzi DRC

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO kwa ushirikiano na taasisi za serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali umeendesha warsha kwa ajili ya kuwafundishia waandishi wa habari kanuni za uandishi wakati wa uchaguzi.

Warsha iliyoendeshwa jumatatu hii mjini Kisangani mashariki mwa DRC imeshirikisha waandishi na viongozi wa vyombo vya habari wapatao 50, huku MONUSCO ikieleza kwamba warsha hiyo imetekelezwa baada ya ripoti kubaini baadhi ya makosa katika uandishi wa habari tangu kutangazwa kwa ratiba ya uchaguzi.

Moja ya kanuni zinazozingatiwa ni kuhakikisha kila mgombea anapata haki sawa ya kutangazwa kwenye vyombo vya habari ambavyo havipaswi kupendelea chama kimoja.

Akihutubia kikao hicho, Naibu Meya wa Kisangani Justin Ramazani Tabora amesisitiza majukumu ya waandishi wa habari wakati wa uchaguzi ili kuelimisha wapiga kura, akikariri kwamba vyombo vya habari vinaweza kufanya kazi kwa uhuru mjini Kisangani.