Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM waitaka Burundi iruhusu wachunguzi wa kimataifa kuingia

UM waitaka Burundi iruhusu wachunguzi wa kimataifa kuingia

Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari, Adama Dieng, ameitaka serikali ya Burundi iruhusu wachunguzi wa kimataifa kuingia nchini humo ili wachunguze ukiukwaji wa haki za binadamu unaoendelea, na uwezekano wa kuwepo wachochezi kutoka nje ya Burundi wanaochangia kwa kutoa rasilmali. Taarifa kamili na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Akiongea kutoka kwenye Ofisi ya Haki za Binadamu mjini Geneva, Uswisi, Bwana Dieng amesema wadau wa kikanda wana jukumu kubwa la kutimiza katika upatanishi na kuzuia ukiukwaji mkubwa zaidi wa haki za binadamu nchini Burundi, akiitaka Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa macho zaidi.

“Bila shaka tuna Rais Museveni wa Uganda ambaye ni mpatanishi, lakini sidhani kama kutakuwa na ufanisi wowote hapa. Tunachohitaji ni labda kumtuma mtu mwingine, ama kutoka Kenya, kumsaidia rais wa Uganda. Tumakinike zaidi, kwani Uganda wana uchaguzi- na hivi sasa wanajali zaidi katika uchaguzi wao”.

Bwana Dieng amesema, ingawa hataki kusema kuna wachochezi kutoka nje, ni bora kuchunguza uwezekano wa hilo. Amesema kinachohitajika zaidi ni kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu na kuwawajibisha wanaoutekeleza..

“Pasipokuwa na uwajibikaji kama njia ya kukomesha kinachoendelea Burundi, hatutaona mwisho wa tanuri hili, na tutakuwa na suluhu hafifu. Ni muhimu kuhakikisha kuwa ukwepaji sheria hauendelezwi Burundi.”