Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Syria: hatari ya wakimbizi yaongezeka sana tangu 2014

Syria: hatari ya wakimbizi yaongezeka sana tangu 2014

Tathmini ya kila mwaka ya hali ya wakimbizi wa Syria imeonyesha kuwa wakimbizi hao wanaishi katika hali ngumu na hatarishi zaidi kuliko walivyokuwa mwaka 2014.

Ripoti ya tathmini hiyo ya mwaka 2015 iliyozinduliwa leo na mashirika ya Umoja wa Mataifa yakiwemo la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, la mpango wa chakula, WFP na la kuhudumia watoto, UNICEF, imeonyesha kuwa takriban asilimia 70 ya wakimbizi wa Syria walioko nchini Lebanon wanaishi katika hali iliyo chini ya kiwango cha Lebanon cha umaskini uliokithiri, cha dola tatu na senti themanini kwa siku.

Ripoti inasema kiwango cha hali ngumu kimeongezeka kwa asilimia 49 tangu mwaka 2014, huku mwakilishi wa UNHCR nchini Lebanon, Mireille Girard akisema wakimbizi hao wanahitaji mshikamano na usaidizi endelevu wa kimataifa, na pasi usaidizi kama huo, watatumbukia katika umaskini mkubwa hata zaidi.