Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama lalaani shambulio la bomu Afghanistan.

Baraza la usalama lalaani shambulio la bomu Afghanistan.

Wajumbe wa baraza la usalama wamelaani vikali shambulio la kigaidi la Desemba 2, karibu na uwanja wa ndege uitwao Bagram nchini Afghanistan ambapo takribani watu sita kutoka Marekani wamefariki huku wengine kadhaa wakijeruhiwa.

Kundi la wanamgambo wa Taliban wamedai kuhusika na shambulio hilo ambapo wajumbe wa baraza la usalama wameelezea rambirambi zao za dhati kwa familia za waathiriwa, watu na serikali ya Marekani na Afghanistan. Pia wamewatakia uponyaji wa haraka.

Wajumbe wamekariri sikitiko lao kuhusu tishio linalowekwa na vikundi vyenye msimamo mkali ikiwemo Taliban, Al-Qaida, ISIL (Da’esh) na washirika wao waliojihami kwa raia, ulinzi wa nchi, vikosi vya usalama, na uwepo wa jumuiya ya kimataifa nchini Afghanistan.

Wamesisitiza umuhimu wa kuwafikisha mahakamani watekelezaji, waandaji, wawezeshaji na wafadhili wa tukio hilo la kutisha na kutaka serikali kulingana na wajibu wao katika sheria za kimataifa na azimio la baraza la usalama, kushirikiana kikamilifu na mamlaka ya Afghanistan katika kufanikisha mchakato wa kisheria.