Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nyuklia yatarajiwa kuokoa uzalishaji wa ndizi

Nyuklia yatarajiwa kuokoa uzalishaji wa ndizi

Teknolojia za kinyuklia huenda zitaponesha ugonjwa wa kuvu unaoathiri uwepo wa ndizi tamu aina ya Cavendish.

Hii ni kwa mujibu wa Shirika la nishati ya atomiki duniani, IAEA, ambalo wiki iliyopita limeitisha mkutano wa watalaam mjini Vienna Austria kwa ajili ya kuanzisha utafiti kuhusu jinsi ya kuimarisha uzalishaji wa ndizi zitakazostahmili ugonjwa huo na hivyo kutunza riziki na uhakika wa chakula kwa mamilioni ya watu duniani.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo, IAEA imeeleza kuanzisha mradi mpya wa utafiti ambao utatumia teknolojia ya nyuklia kwa ajili ya kubuni aina mpya za ndizi na kahawa zitakazostahamili magonjwa. Tayari aina bora ya ngano imezalishwa nchini Kenya mwaka 2014 kwa ushirikiano na IAEA.

Kwa mujibu wa IAEA, kuvu inayoathiri ndizi imeanza kuenea Asia, Australia, Mashariki ya Kati na hivi karibuni maeneo kadhaa ya Afrika.