Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtaalam wa UM atolea wito uchaguzi wa amani, haki na uhuru CAR

Mtaalam wa UM atolea wito uchaguzi wa amani, haki na uhuru CAR

Mtaalam huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR,  Marie-Thérèse Keita Bocoum, amewapa heko takriban watu milioni mbili nchini humo waliojiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa urais na ubunge, akiwahimiza kushiriki katika uchaguzi huo muhimu wa Jumapili, Disemba 27.

Akikariri umhimu wa uchaguzi huo kwa mustakhbali wa CAR, Bi Keita Bocoum amesema uchaguzi huo unapaswa kuwa hatua kubwa kwa nchi hiyo hatimaye kuondokana na machafuko na chuki, na kufungua njia ya maridhiano na kujijenga tena.

Aidha, Bi Keita Bocoum ameeleza kusikitishwa na shambuluizi la Disemba 17 dhidi ya wagombea wa urais, na kutoa wito hatua zichukuliwe mara moja kuwakabili waliokitekeleza kitendo hicho kisheria.

Amesema kuheshimu haki za binadamu wakati wa mchakato wa uchaguzi ujao ni kiungo muhimu cha kuhakikisha kuwa upigaji kura unafanyika kwa njia huru, salama, mara kwa mara, na kwamba unadhihirisha matakwa ya watu wa CAR.