Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi ya makombora kutoka eneo la UNIFIL yanatia hofu:Ban

Mashambulizi ya makombora kutoka eneo la UNIFIL yanatia hofu:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon amesema anatiwa wasiwasi na kitendo cha jana cha kuvurumisha makombora ndani ya eneo la mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon UNIFIL, yakitokea eneo la Al-Hinniyah, katikati ya Tyr kuelekea Israel jambo ambalo ni ukiukaji mkubwa wa azimio 1701 la mwaka 2006.

Ban amesema pia amebaini mashambulizi ya ulipizaji kisasi yaliyofanywa na vikosi vya ulinzi vya Israel nchini Lebanon katika eneo Zibqin. UNIFIL kwa ushirikiano na jeshi la Lebanon inachunguza hali iliyopelekea kufanyika kwa tukio hilo.

Katibu Mkuu analaani ukiukwaji wa aina yoyote wa azimio 1701 la 2006 na kuzitaka pande zote  kushirikiana na UNIFIL ili kuzuia hali kuwa mbaya zaidi.

Umoja wa Mataifa umedhamiria kuendelea kufanya kazi kwa karibu na pande zote kuhakikisha hali ya utulivu iliyoko Kusini mwa Lebanoni inaendelea.