Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO na DfID zaimarisha ushirikiano wao kuokoa sekta ya chakula

FAO na DfID zaimarisha ushirikiano wao kuokoa sekta ya chakula

Shirika la Chakula na Kilimo Duniani, FAO na idara ya maendeleo ya kimataifa ya Uingereza, DfID, wameingia mkataba mpya unaolenga kuimarisha ushirikiano zaidi kati ya pande mbili hizo.

Mkurugenzi Mkuu wa FAO José Graziano da Silva amesema hatua hiyo mpya inazingatia kuwa taasisi hizo mbili zina dira moja ya kuwa na dunia ambayo kwayo jamii zina uhakika wa chakula na rasilimali zao zinalindwa na kutumiwa kiuendelevu.

Bwana da Silva amesema makubaliano hayo mapya yanaweka mfumo wa kisheria wa ushirikiano kati ya pande mbili hizo kuelekea mriadi mpya kwa kipindi cha miaka angalau 10 na itawezesha miradi kujadiliwa kwa ujumla badala ya pande moja moja kuwasilisha miradi yake kwa DfID.

Amesema Uingereza kupitia DfID imekuwa mstari wa mbele kusaidia harakati za FAO akitolea mfano kusaidia mikakati ya usalama wa chakula Zimbabwe na kupitia kuongeza tija katika uzalishaji mazao na kusaka masoko mapya.

Kati ya mwaka 2012 na 2015, serikali ya Uingereza imekuwa ya tatu kwa kuipatia FAO usaidizi ambapo imechangia zaidi ya dola Milioni 360 katika miradi.