Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama lasikitishwa kuendelea kwa machafuko Burundi

Baraza la usalama lasikitishwa kuendelea kwa machafuko Burundi

Wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa  wamesisitiza kusikitishwa na kuendelea kwa machafuko nchini Burundi, kuongezeka kwa visa vya uvunjifu wa haki za binadamu na misuguano ya kisiasa.

Taarifa ya baraza hilo iliyotolewa Jumamosi inasema kuwa wajumbe wa baraza wamelaani vitendo hivyo bila kujali vimetekelezwa na nani na kwamba vinasababisha madhila ya kibinadamu.

Taarifa ya baraza la usalama kadhalika imelaani matamko ya kichochezi yaliyotolewa na viongozi wa kisiasa wa Burundi, kulaani mashambulizi dhidi ya vituo vya kijeshi mjini Bujumbura na vijijini, pamoja na mauaji yanayotekelezwa baada ya mashambulizi na kutaka wahusika wawajibishwe kisheria.

Baraza la usalama limekariri kupitishwa kwa azimio la baraza la haki za binadamu la kulaani uvunjifu na ukiukwaji wa haki za binadamu nchini humo, unatoekelezwa na wadau wa kisiasa ambapo azimio hilo liliamua kutuma ujumbe wa wataalamu ili kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu.