Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Azimio la kihistoria lapitishwa kuhusu Syria

Azimio la kihistoria lapitishwa kuhusu Syria

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo limepitisha azimio la kihistoria kuhusu Syria linalosisitiza kwamba suluhu ya pekee kwa mzozo wa Syria ni ya kisiasa. Azimio hilo limeziomba pande zote kuelewana na kuunda serikali jumuishi ya mpito ikilinda umoja wa nchi hiyo pamoja na haki za raia wote bila kubagua kundi lolote kwa misingi ya kidini au kikabila.

Akihutubia kikao hicho, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema mzozo wa Syria umeanza na maombi ya raia wakitaka mabadiliko ya kisiasa, ukiendelea kuchochewa na mivutano ya ndani na ya kimataifa hadi kwenye baraza la usalama lenyewe.

Ametoa mapendekezo manne kwa pande zinazohusika na mzozo yakiwa ni kusitisha matumizi ya silaha dhidi ya raia, kuruhusu usambazaji wa misaada ya kibinadamu, kusitisha mashambulizi dhidi ya vituo vya afya, na hatimaye kuachilia huru wafungwa wote, akisema

(Sauti ya Bwana Ban)

“Raia wa Syria wameshateseka vya kutosha. Nawomba kuonyesha dira na uongozi katika kukabiliana na tofauti zenu. Fursa ya amani imeibuka, wajibu wenu ni kuichukua.”

Kwa upande wake, waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema

(sauti ya John Kerry)

Baraza hili linapeleka ujumbe dhahiri kwa pande zote husika kwamba wakati ni sasa wa kukomesha mauaji nchini Syria na kuweka msingi kwa ajili ya serikali ambayo kwa muda mrefu watu wanaoteseka wanaweza wanawaza kuisaidia. Baada ya miaka minne na nusu ya vita hii ni mara ya kwanza tumeweza kukutana pamoja katika Umoja wa Mataifa katika Baraza la Usalama kukubaliana mwelekeo wa kusonga mbele. Wakati huo, msyria moja kati ya 20 ameuawa au kujeruhiwa, mmoja kati ya watano ni mkimbizi, moja kati ya wawili amekuwa mkimbizi wa ndani."