Watu milioni 2.4 wanahitaji msaada Libya:OCHA

Watu milioni 2.4 wanahitaji msaada Libya:OCHA

Kufuatia kutiwa saini kwa muafaka wa kisiasa wa Libya huko Morocco Alhamisi, shirika la Umoja wa mataiofa la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA limeelezea hali halisi ya kibinadamu Libya na kuainisha mipango ya usaidizi wa hadi disemba 2016.

Mipango hiyo itatoa msaada wa kibinadamu kwa watu milioni 1.3 kati milioni 2.4 wanaokadiriwa kuhitaji msaada. OCHA inasema inahitaji dola milioni 165.5 ili kukidhi mahitaji ya watu hao. Jens Learke ni msemaji wa OCHA.

(SAUTI YA JENS LEARKE)

"Huduma za msingi zimedhoofika, hasa mfumo wa afya unakaribia kuteketea kwa sababu ya ukosefu wa upungufu wa wauguzi na vifaa vya afya. Takribani  asilimia 20 ya hospitali nchini Liyba zimefungwa wakati ambapo watu wapatao milioni mbili wanahitaji usaidizi wa afya. Malaki ya watu wanaishi kwenye mazingira hatarishi sana." 

Msaada una malengo matatu makubwa , kwanza ni kuokoa maisha na kuboresha hupatikanaji wa mahitaji ya lazima, pili kuwalinda walio katika hatari Zaidi ikiwemo wanawake na watoto na mwisho ni kuboresha ujasiri wa jumuiya zilizoathirika.