Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR kutoa muongozo wa kuwalinda wakimbizi

UNHCR kutoa muongozo wa kuwalinda wakimbizi

Shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR leo linatoa muongozo  wenye lengo la kuzisaidia nchi kukabiliana na hatari za usalama huku zikizingatia viwango muhimu vya kuwalinda wakimbizi.

Mapendekezo ya muongozo huo yamo katika nyaraka iliyowasilishwa na naibu kamishina kwa ajili ya ulinzi kwa wakimbizi Volger Türk mbele ya mkutano baina ya serikali mbalimbali.

Muongozo huo unadai kwamba usalama wa kitaifa na ulinzi kwa wakimbizi havitofautiani na kutoa wito wa mtazamo utakaohakikisha malengo ya mambo haya mawili yanatimizwa. Adrian Edward ni msemaji wa UNHCR

(SAUTI YA ADRIAN EDWARD)

"Kuhusu suala la kudhibiti mipaka tunaelewa umuhumu wa nchi kuimarisha usalama katika milango mfano ukaguzi kupitia vifaa vya kisasa, mapendekezo ni kuhakikisha hatua hizi zinafanywa kwa umakini na kufuata sheria pamoja na kuepuka ubaguzi wa utaifa, ukabila au udini."