Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Angazia nuru janga la wahamiaji:IOM

Angazia nuru janga la wahamiaji:IOM

Ikiwa leo ni siku ya wahamiaji duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesihi jamii ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti na za kibinadamu katika kushughulikia janga la wahamiaji ulimwenguni.

Ametoa kauli hiyo wakati huu ambapo mwaka 2015 pekee umeshuhudia zaidi ya watu Elfu Tano wakipoteza maisha yao katika safari za kwenda kusaka usalama wa maisha yao, wengi wao wakielekea barani Ulaya wakitokea Afrika na Mashariki ya Kati.

Katika ujumbe wake Ban amesema ni lazima kupanua wigo wa njia salama za uhamiaji ikiwemo familia kuungana, kusaka ajira na elimu akisihi nchi zote kutia saini mkataba wa kimataifa wa ulinzi wa haki za wahamiaji,wafanyakazi na familia zao.

Nalo shirika la kimataifa la uhamiaji limetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuungana hii leo na kuwasha mshumaa kukumbuka waliopoteza maisha yao baharini au jangwani wakiokoa maisha.

William Swing ni Mkurugenzi Mkuu wa IOM

(Sauti ya William)

Wahamiaji wanasonga, na dunia inawahitaji. Lakini dunia pia inatahiji uongozi ili kuwaongoza kwa usalama, uhakika na kisheria. Wakati umefika kwa jamii zilizokomaa kuonyesha kuwa manufaa ya pande zote hizo mbili yanafanikiwa. Ni kweli kuna giza. Lakini sote tuna nuru kidogo. Tuangazie nuru hiyo na tuwache iangaze.”