Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watoto 380,000 hawako shuleni Mali, UNICEF yachukua hatua

Zaidi ya watoto 380,000 hawako shuleni Mali, UNICEF yachukua hatua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limechukua hatua kuwarejeshea haki yao ya kupata elimu, zaidi ya watoto 380,000 huko kaskazini mwa Mali ambao hawajaenda shuleni, licha ya muhula mpya wa masomo kuanza miezi mitatu iliyopita.

Katika taarifa yake, UNICEF imesema watoto hao wenye umri wa kati ya miaka Saba hadi 15 wanashindwa kwenda shule kutokana na ukosefu wa usalama kaskazini mwa Mali ikiwa ni miaka karibu minne tangu usalama kuzorota kwenye eneo hilo.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Mali, Fran Equiza amesema mzozo umesababisha shule zaidi ya 280 kufungwa, ikitolea mfano eneo la Kidal ambapo asilimia 79 ya shule zote zimefungwa kati ya hizo kwa miaka mitatu mfululizo, nyingine zimeporwa vifaa huku hata zile zilizofunguliwa watoto wana hofu kutokana na ukosefu wa usalama.

Kwa mantiki hiyo, UNICEF imeanzisha kampeni ya kila mtoto ni muhimu ikiwa na mambo muhimu matatu, fursa za mafunzo  na vifaa kwa walimu Elfu Mbili, watoto Laki Moja kupatiwa vifaa vya kujifunzia sanjari na vifaa vya kuelimishia watoto kuhusu ujenzi wa amani.

Halikadhalika kampeni hiyo itahusisha mafunzo kwa njia ya redio hasa kwa watoto ambao hawako shuleni pamoja na ukarabati wa shule zilizoharibiwa.

Mwakilishi huyo wa UNICEF amesema ndoto ya ujenzi wa mustakhbali bora zaidi wa watoto wa Mali inategemea hatua zinazochukuliwa sasa.