Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO yataka ushirikiano zaidi na jeshi la DRC

MONUSCO yataka ushirikiano zaidi na jeshi la DRC

Ushirikiano wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC MONUSCO na jeshi la kitaifa la DRC FARDC ni muhimu ili kuhakisha operesheni za kijeshi zinafanyika kwa kuzingatia maslahi ya wananchi.

Hii ni kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa kikosi cha MONUSCO, Jenerali Jean Baillaud, ambaye jumatano hii ametembelea mji wa Lubumbashi, kwenye jimbo la Katanga nchini DRC.

Kwenye taarifa yake MONUSCO imesema wakati wa ziara yake Jenerali Jean Baillaud amekutana na viongozi wa kisiasa na kijeshi wa Katanga ambao wameelezea wasiwasi wao kuhusu hali ya usalama kwenye eneo lililo karibu na mbuga ya Upemba ambako waasi wa Mai-Mai hushambulia raia.

Aidha viongozi hao wameiomba MONUSCO isaidie kupambana na waasi hao wakisisitiza kwamba ushirikiano wao na FARDC umesaidia jeshi wa DRC kuheshimu zaidi haki za binadamu.

Kwa upande wake Jenerali Baillaud amekariri kwamba ushirikiano wa MONUSCO na FARDC huleta ufanisi zaidi.