Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza Saudia unatia hofu:UM

Ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza Saudia unatia hofu:UM

Mtaalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa mataifa David Kaye leo ameelezea hofu yake kuhusu kuongezeka kwa ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza nchini Saudi Arabia. Amesema amebaini mlolongo wa adhabu dhidi ya watu wanaoelezea maoni yao, wakiwemo watetezi wa haki za binadamu na wamiliki wa blogi, Raif Badawi na Mikhlif al Shammai, pamoja na mshairi Asharaf Fayadh.

Bwana Kaye ambaye ni mwakilishi maalumu wa haki ya uhuru wa maoni na kujieleza ,amesema wakati dunia ikijitahidi kukabiliana na mifumo mibaya ya ghasia uongozi wa serikali kila mahali lazima uepuke kukandamiza uhuru wa kujieleza, hususani dhidi ya wale wanaochagiza kuvumiliana, heshima na haki za binadamu.

Ameongeza kuwa waandishi kadhaa na wasanii wameadhibiwa vikali kwa kuelezea yale wanayoyaamini nchini Saudi Arabia. Mfano bwana Badawi ambaye alipewa tuzo ya haki za binadamu, alihukumiwa kwenda jela mwaka 2014 na Januari kucharazwa  bikoko 50 hadharani.

Mwakilishi huyo ameitaka serikali ya Saudia kupitia upya sheria zake na kuruhusu uhuru wa kujieleza kwa wote ikiwemo wasanii na watetezi wa haki za binadamu, na apia amelendelea na nia yake ya kutaka kuzuru taifa hilo ili kjadili Zaidi suala hilo.