Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sera za uvumbuzi Afrika zaweza kuboreshwa: UNCTAD

Sera za uvumbuzi Afrika zaweza kuboreshwa: UNCTAD

Ripoti ya kamati ya Umoja wa Mataifa ya biashara na maendeleo, UNCTAD kuhusu teknolojia na uvumbuzi mwaka 2015,  inasema mambo mengi zaidi yaweza kufanywa ili kusababisha sera za uvumbuzi barani Afrika kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo.

Ikiwa na jina kuwezesha sera za uvumbuzi kwa ajili ya maendeleo ya viwanda, ripoti hiyo iliyotolewa leo mjini Geneva, inasema kuwa licha ya kwamba nchi zinazoendelea zimeuza nje bidhaa za teknolojia kwa asilimia 52 mwaka jana, na kuongeza kwa asilimia 18 katika mauzo tangu mwaka 2000 bado bara hilo linasalia nyuma.

Pia ripoti hiyo imebaini kuwa ugumu wa mikakati ya kuratibu sera za teknolojia na uvumbuzi, ni moja ya sababu na kwamba hata nchi za Afrika zinazotumia fedha nyingi katika utafiti wa maendeleo hazimudu kuuza nje bidhaa za teknolojia za  kiwango cha juu na cha kati.

Ikitolea mifano ya viwanda na teknolojia ya sayansi,  ripoti hiyo imezitaja nchi kama vile Tanzania, Ethiopia na Nigeria na kushauri kuwa tafsiri za sera, mipango  na utekelezaji ni muhimu katika kufikia mafanikio ya tekenoljia kufanya kazi.