Skip to main content

Tumejiandaa kama kutakuwepo na wimbi la wakimbizi: UNHCR Tanzania

Tumejiandaa kama kutakuwepo na wimbi la wakimbizi: UNHCR Tanzania

Nchini Tanzania, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema hadi sasa hakuna mabadiliko katika idadi ya wakimbizi wanaoingia nchini humo kutoka Burundi, lakini limejiandaa iwapo kuzorota kwa usalama kutasababisha ujio mkubwa.

Mwakilishi mkazi wa UNHCR nchini Tanzania Joyce Mends-Cole ameiambia idhaa hii wanachofanya sasa..

(Sauti ya Mends-Cole)

“Tunawasiliana na UNHCR Burundi na tumeomba wenzetu walioko Makamba iwapo wataona kama kuna wakimbizi wengi kuliko tunaopokea sasa! Kwa sasa ni angalau wakimbizi 200. Kwa siku kwa hiyo tumewasihi watujulishe iwapo kutakuwepo na ongezeko lolote katika jimbo la Makamba au popote pale.”

Amesema wakimbizi wa sasa na hata wakija wapya wanapelekwa katika kambi mpya za Mtandula, na Nduta lakini Karago ambayo serikali  ya Tanzania iliwapatia pia bado ina changamoto kwa kuwa…

(Sauti ya Mends-Cole)

“Mabadiliko ya tabianchi na mmomonyoko wa ardhi, hatuna uhakika ni kwa kiwango gani au hata kama kuna maji na pengine yatakuwa chini sana na itakuwa vigumu na gharama kubwa kuchimba kisima. Tumepata msaada wa mtaalamu wa uchimbaji visima kutoka Uholanzi na bado hajatupatia ripoti. Kwa hiyo hii ndiyo hali halisi, maji ni tatizo kubwa."