Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto 500 hufa kila siku kwa kukosa maji safi Afrika:UNICEF

Watoto 500 hufa kila siku kwa kukosa maji safi Afrika:UNICEF

Watoto takriban 180,000 wa chini ya umri wa miaka mitano hufa kila mwaka ambao ni sawa na watoto 500 kila siku katika nchi za Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara kutokana na maradhi ya kuhara yanayohusishwa na ukosefu wa maji safi, na hali ya usafi (WASH), limesema shirika la kuhudumia watoto UNICEF wakati wa mkutano wa ufadhili wa fedha kwa ajili ya maji na usafi unaofanyika mjini Dakar Senegal.

Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Magharibi na katikati mwa Afrika Manuel Fontaine amesema wakati watoto wanakufa kila uchao, wengine mamilioni wakidumaa na kuongeza mzigo mkubwa katika uchumi , mchakato wa kukabili hali hiyo lazima ushike kasi na kunahitajika sera imara, ufadhili wa kutosha wa fedha na mabadiliko makubwa katika masuala ya kuyapa kipaumbele miongoni mwa walio na mamlaka ya kuchukua hatua.

Hivi sasa karibu nusu ya watu wote duniani ambao hawana fursa ya maji safi ya kunywa wapo Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara na wengine milioni 700 wako katika mazingira machafu.

Mkutano huo wa kwanza kwa Afrika ya Magharibi na Kati , wa kuchagisha fedha kwa ajili ya maji na usafi umeitishwa na UNICEF kwa ushirikiano na serikali ya Senegal na baraza la mawzrili wa maji wa Afrika.