Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano Tokyo kumulika uwekezaji katika kupambana na HIV, TB na Malaria

Mkutano Tokyo kumulika uwekezaji katika kupambana na HIV, TB na Malaria

Mawaziri wa Afya kutoka nchi kadhaa na viongozi wengine katika sekta ya afya, watakutana jijini Tokyo, Japan kuanzia kesho Disemba 16 hadi 17 ili kutafutia mwarobaini changamoto ya ufadhili kwa programu za kuongeza kasi ya kutokomeza VVU, TB na Malaria, na kujenga mifumo dhabiti ya afya inayowezesha utoaji huduma kwa wote.

Mkutano huo unaoandaliwa na mfuko wa kimataifa wa kupambana na HIV, TB na malaria, Global Fund, utawaleta pamoja viongozi kama Bill Gates, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO, Margaret Chan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Tedros Adhanom Ghebreyesus, Waziri wa Canada wa Maendeleo ya Kimataifa, Marie-Claude Bibeau, miongoni mwa wengine.

Kupiga jeki mfuko wa Global Fund kunaenda sambamba na malengo yaliyokubaliwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mnamo Septemba mwaka huu 2015, yenye dhamira ya kupunguza utofauti na kuwezesha mabadiliko jumuishi na endelevu, huku nchi zikijikita katika kufikia utoaji huduma za afya kwa wote.

Utoaji huduma za afya kwa wote umetambuliwa kuwa muhimu katika kumaliza maambukizi ya VVU, TB na malaria, magonjwa yanayoenea hasa kwa sababu ya umaskini na ubaguzi.