Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazungumzo ya amani ya Yemen yameanza leo Uswisi

Mazungumzo ya amani ya Yemen yameanza leo Uswisi

Mazungumzo yanayodhaminiwa na Umoja wa mataifa ya kusaka amani ya kudumu ya mgogoro wa Yemen yameanza leo nchini Uswis. Mazungumzo hayo yanatafuta suluhu ya kudumu ya usitishaji mapigano , kuimarisha hali ya kibinadamu na kurejea kwa Amani na utulivu wa kipindi cha mpito cha kisiasa. Grace Kaneiya na taarifa Zaidi.

(TAARIFA YA GRACE KANEIYA)

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu kwa ajili ya Yemen Ismail Ould Cheikh Ahmed, amewataka wajumbe kuhakikisha wanaheshimu usitishwaji wa mapigano ulioanza sanjari na mazungumzo hayo.

Amesema usitishaji wa mapigano ulioanza leo uwe ni ishara ya kukomesha ghasia za kijeshi na uwe ni kipindi cha mpito kwa hatua ya majadiliano na muafaka.

(SAUTI YA OULD CHEIKH AHMED)

“ Leo nyie ni waamuzi na mbele yenu kuna wajibu wa kihistoria. Je mtatelekeza Yemen na raia wake na kuipeleka nchi katika ghasia na mauaji zaidi, au mtaiweka Yemen mbele, mtarejesha roho nyuma, kufufua mamlaka za serikali na kuhakikishia watu wa Yemen wanaweza kuishi maisha ya utu wanayostahili?"

Mazungumzo hayo ya Amani yanahudhuriwa na wawakilishi na washauri 24 , na Umoja wa mataifa unashirikiana na ujumbe huo kuandaa makubaliano yatakayoimarisha hali ya kibinadamu nchini Yemen.