Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila mwaka hali ya watoto vitani inazidi kuzorota- Zerrougui

Kila mwaka hali ya watoto vitani inazidi kuzorota- Zerrougui

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kuhusu watoto katika mizozo ya silaha, Leila Zerrougui, amesema leo kuwa mwaka 2015 umekuwa mbaya sana kwa watoto katika maeneo yenye migogoro ya silaha duniani.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva kuhusu hali ya watoto katika mizozo ya silaha mwaka 2015, Bi Zerrougui amesema tangu alipoteuliwa katika wadhfa huo mwaka 2012, hali hiyo imekuwa ikizorota hata zaidi kila mwaka.

Bi Zerrougui amesema mizozo sita tofauti mikuu, ikiwemo ya Iraq, Syria, Yemen, Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Afghanistan, na kuendelea kwa mizozo ya zamani, imechangia hali kuwa ngumu hata zaidi kwa watoto.

Kuna maelfu ya watoto waliouawa au kujeruhiwa, shule zimeshambuliwa, maelfu ya watoto katika maeneo mengi wameingizwa vitani. Kwa mfano hali Kaskazini mwa Nigeria na Ziwa Chad, ambapo Boko Haram wanatenda ukatili mkubwa- watoto sio tu wanaathiriwa, lakini wanalengwa moja kwa moja. Wasichana wadogo wanatumia katika mashambulizi ya bomu ya kujitoa mhanga.”