Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pande kinzani Sudan Kusini malizeni tofauti zenu:UNMISS

Pande kinzani Sudan Kusini malizeni tofauti zenu:UNMISS

Miaka miwili tangu kuanza kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNMISS umesema ni kipindi kirefu mno lakini wanachofanya ni kuhakikisha mkataba wa amani unatekelezwa.

Akihojiwa na Radio Miraya iliyo chini ya UNMISS, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja w Mataifa nchini humo Ellen Margrethe Loej  amesema mkataba ulitiwa saini na pande kinzani ambazo ni serikali na kikundi cha SPLM/A cha upinzani lakini changamoto za utekelezaji zinatofautiana na mtazamo wa kila upande hivyo amesema.

(Sauti ya Margaret)

“Waondoe vikwazo hivyo. SPLM/A upinzani itume ujumbe wao Juba, ishiriki mikutano ya mfumo wa ufuatiliaji pamoja-JEM, majadiliano ya utekelezaji wa mkataba na usitishaji mapigano, na uanzishwaji wa polisi wa pamoja.”

Kuhusu usaidizi wa kibinadamu, Bi. Loej ambaye pia ni mkuu wa UNMISS amesema watoa huduma wanajitahidi lakini wana changamoto ikiwemo kupata fedha na pia kushindwa kufikia wahitaji kutokana na mvua na ukosefu wa usalama.

Wakati huo huo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa na kikao kuhusu Sudan Kusini ambapo limeongeza muda wa UNMISS hadi tarehe 31 Julai mwaka 2016.