Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Burundi vita vya wenyewe kwa wenyewe vyanukia:OHCHR

Burundi vita vya wenyewe kwa wenyewe vyanukia:OHCHR

Wakati Baraza la haki za binadamu likijiandaa kuwa na mjadala kuhusu Burundi siku ya Alhamisi, hii leo kamishna mkuu wa haki za binadamu ameeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu janga linalozidi kuchipuka kila uchao nchini humo. Taarifa zaidi na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Msemaji wa ofisi ya haki za binadamu Cécile Pouilly akizungumza Geneva, Uswisi amegusia mauaji ya Ijumaa kwenye mji mkuu Bujumbura na misako iliyofanywa na vikosi vya usalama katika vitongoji vya Musaga na Nyakabiga.

Kufuatia misako hiyo mamia ya wanaume walikamatwa, baadhi  yao kupelekwa maeneo yasiyojulikana hivyo amesema..

(Sauti ya Cécile)

Kutokana na mfululizo wa matukio ya umwagaji damu, nchi hii inaonekana kuchukua mwelekeo wa kuwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, na hofu imefikia kiwango cha juu Bujumbura. Kamishna Mkuu anasihi pande zote kwenye mzozo wa sasa wakiwemo viongozi wa kisiasa na mamlaka za juu za serikali kuchukua hatua wawezazo kusitisha ghasia mbaya zinazoendelea, na washiriki mashauriano ya dhati.”

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR hadi sasa raia zaidi ya 220,000 wa Burundi wamesajiliwa kama wakimbizi katika nchi jirani za Rwanda, DR Congo, Tanzania na Uganda kutokana na ghasia zilizokumba nchi hiyo.