Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wa haraka wa huduma za afya kwa watu milioni 15 wahitajika Yemen:WHO

Msaada wa haraka wa huduma za afya kwa watu milioni 15 wahitajika Yemen:WHO

Shirika la afya duniani WHO na washirika wake wametoa ombi la dola milioni 31 ili kuhakikisha kuendelea kwa huduma za afya kwa watu takribani milioni 15 walioathirika na vita vinavyoendelea nchini Yemen.

Fedha hizo zinahitajika haraka wakati huu ambapo mfumo wa afya wa Yemen umesambaratika na kuwaacha mamilioni ya watu bila huduma na dawa wanazohitaji. Kwa mujibu wa mkurugenzi wa kanda ya Mashariki mwa Mediteraniani wa WHO Dr Ala Alwan shirika hilo linaomba wahisani ili kukidhi mahitaji ya haraka ya kibinadamu kwa majeruhi, mama wajawazito, watoto wenye utapia mlo na wazee ambao ndio waathirika wakubwa wa kusambaratika kwa mfumo huo.

WHO imesema ikipata fedha za kutosha itapunguza hatari ya milipuko ya magonjwa , itagawa dawa zitakazoasaidia kuokoa maisha, na kuwapa chanjo watoto kuepuka vifo vinavyoweza kuzuilika. Fedha hizo zikipatikana zitajikita katika maeneo matatu muhimu, kutoa tiba kwa majeruhi, kutibu maradhi sugu na shughuli za chanjo kuzuia milipuko ya magonjwa.