Skip to main content

Nchi zimefanya chaguo la kihistoria kwa Mkataba wa Paris- Ban

Nchi zimefanya chaguo la kihistoria kwa Mkataba wa Paris- Ban

Mkataba wa Paris unaweza kuunufaisha ubinadamu wote kwa miaka mingi na vizazi vijavyo. Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, akikutana na waandishi wa habari jijini New York, kufuatia kupitishwa kwa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, uliosainiwa jijini Paris Ufaransa, mwishoni mwa wiki iliyopita.

Katika mkataba huo wa Paris, nchi zimeahidi kudhibiti viwango vya ongezeko la joto duniani na kuhakikisha hakizidi nyuzi joto mbili kwa kipimo cha Selsiasi, na kuendeleza msukumo wa kulenga kufikia nyuzi joto moja na nusu kwenye kipimo hicho.

Ban amesema Mkataba wa Paris ndiyo hatua muhimu zaidi katika kipindi cha miaka mingi, katika kutimiza wajibu wa Katiba ya Umoja wa Mataifa, ya kulinda vizazi vijavyo.

“Nchi zote duniani zimefanya chaguo la kihistoria. Zimeamua kwa kauli moja kufanya kazi pamoja, kukabiliana na changamoto kuu ya nyakati zetu. Mkataba wa Paris ni ushindi kwa watu, kwa maslahi ya wote na kwa ushirikiano. Ni sera bima ya afya ya sayari dunia.

Katibu Mkuu amesema mkataba wa Paris ni tukio la muhimu katika juhudi za kimataifa za kuweka mustakhbali salama, endelevu na wenye ufanisi.

“Kwa mara ya kwanza, kila nchi duniani imeahidi kudhibiti uchafuzi, kuimarisha uthabiti na kuchukua hatua kimataifa na kitaifa, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Nchi zimetambua kuwa maslahi ya kitaifa yanazingatiwa vyema kwa kuchukua hatua kwa maslahi ya wote.

Aidha, Ban amesema mkataba wa Paris ni ishara dhahiri kuwa kubadili uchumi wa kimataifa ili uwe wenye uchafuzi mdogo na ukuaji wenye uthabiti, tayari kumeanza.