Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali nchini Burundi ni tete, yatia hofu- Benomar

Hali nchini Burundi ni tete, yatia hofu- Benomar

Hali nchini Burundi inatia hofu, kiwango cha ghasia kikiwa kimefikia upeo mpya, amesema Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Burundi, Jamal Benomar. Taarifa kamili na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Bwana Benomar amesema hayo wakati akiihutubia Kamisheni ya Ujenzi wa Amani Burundi, katika mkutano uliowaleta pamoja wajumbe wa Baraza la Usalama na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Bwana Benomar amesema taifa la Burundi lilikuwa na matumaini makubwa miaka kumi iliyopita baada ya miaka mingi ya misukosuko, lakini sasa kuna picha ya kutia hofu, kutokana na matukio ya hivi karibuni, yakiwemo mauaji holela, akitaja mfano wa mashambulizi yaliyotokea mwishoni mwa wiki iliyopita.

Amesema kiwango cha machafuko kilichoshuhudiwa wiki chache zilizopita hakijawahi kuonekana. Kwa mantiki hiyo, ameeleza kinachopaswa kufanywa ili kuidhibiti hali

“Kwetu sisi tunachoona kama cha kipaumbele ni kuunga mkono juhudi zote za wadau wa kitaifa na kimataifa katika kuzuia hali ya machafuko kuzorota zaidi, na hili linaweza kutimia tu kupitia mchakato fanisi na jumuishi wa kisiasa.”