Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto 710,000 wakimbizi kupata fursa ya elimu ya msingi: UNHCR/EAC

Watoto 710,000 wakimbizi kupata fursa ya elimu ya msingi: UNHCR/EAC

Mfuko wa mpango wa kimataifa wa elimu zaidi ya yote EAC na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR wanazindua ushirika mpya wa miaka miatatu  ambao utatoa fursa ya elimu kwa watoto 710,000 walioathirika na vita na kulazimika kuwa wakimbizi barani Afrika, Asia na Mashariki ya Kati.

Ikiwa ni katika kuendeleza ushirikiano ambao tayari umeshawapa watoto Zaidi ya 260,000 fursa ya elimu ya msingi tangu mwaka 2012  ufadhili mpya wa EAC utaendelea kuunga mkono elimu ya watoto hawa na kusaidia kuandikisha wengine 450,000 mashuleni katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Karibu nusu ya watakaofaidika na mpango huo wanatarajiwa kuwa watoto waliotawanywa na machafuko nchini Syria na waliosalia ni kutoka Chad, Ethiopia, Iran, Kenya, Malaysia, Pakistan, Rwanda, Sudan,  Sudan Kusini, Uganda na Yemen.

Vita na mauaji imewalazimu mamilioni ya watu kukimbia makwao , ambapo watu takriban milioni 60 walikimbia kusaka usalama kufikia mwisho wa mwaka 2014, huku watoto wakiwa ni nusu ya wakimbizi wote duniani wakikabiliwa na hatari kubwa.