Makubaliano ya Minsk ndiyo njia bora ya kutanzua mzozo wa Ukraine- Eliasson
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson, ameliambia Baraza la Usalama la Umoja huo kuwa makubaliano ya Minsk bado ndiyo yanayotoa fursa na njia mwafaka zaidi katika kupatia suluhu mzozo wa Ukraine, na kwamba makubaliano hayo ni lazima yatekelezwe kikamilifu.
Bwana Eliasson amesema hayo wakati wa mkutano wa Baraza la Usalama leo, ambao umeangazia hali nchini Ukraine, miaka miwili tangu kuzuka machafuko nchini humo.
Naibu huyo wa Katibu Mkuu amesema, pande zote kinzani katika mzozo wa Ukraine ni lazima zifanye kazi bila kuchelewa, kuelekea suluhu la kisiasa la kudumu, na kwamba utashi mkubwa wa kisiasa na kulegeza misimamo ni lazima vidhihirishwe na wahusika wote.
“Mamilioni ya wanawake, watoto, wazee na watu wenye ulemavu wameathiriwa moja kwa moja pande zote za mzozo. Kuchelewesha suluhu zaidi kutamaanisha mateso zaidi kwa watu wengi hata zaidi, ambao sasa wanatumainia amani wakati wa msimu wa mapumziko na siku kuu.”
Aidha, Bwana Eliasson amesisitiza haja ya kuongeza jitihada ili usifanyike tena mkutano mwingine wa Baraza la Usalama mwakani, kuadhimisha miaka mitatu tangu mzozo huo kuanza.