Ban alaani mashambulizi kwenye kambi Bujumbura
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani mashambulizi yaliyofanywa na watu wasiojulikana kwenye kambi moja ya kijeshi huko Bujumbura, Burundi.
Taarifa ya msemaji wake imemkariri akisema vitendo hivyo vya ghasia vinaweza kusababisha ukosefu zaidi wa utulivu nchini humo.
Katibu Mkuu amesihi uongozi wa vikundi hivyo na mamlaka za taifa kujizuia kufanya vitendo vitakavyochochea zaidi ghasia au kulipiza kisasi akisema yeyote ambaye atahusika na kuagiza ukiukwaji wa haki za binadamu atawajibishwa.
Halikadhalika ametoa wito kwa wadau wa kitaifa nchini Burundi kuzingatia hseria akisihi mamlaka za kiserikali kusaidia kuweka mazingira yatakayowezesha kuwepo kwa mashauriano shirikishi yatakayoondoa changamoto za kisiasa zinazokumba nchi hiyo kwa sasa.
Ban amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake uko tayari kusaidia jitihada zozote za kusuluhisha mzozo Burundi kwa amani.