Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 20 tangu Copenhagen, Kenya yazungumzia mafanikio

Miaka 20 tangu Copenhagen, Kenya yazungumzia mafanikio

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mjadala wa wazi kuhusu miaka 20 tangu kufanyika kwa mkutano wa dunia kuhusu maendeleo ya jamii, WSSD huko Copenhagen, Denmark.

Mkutano huo ulileta pamoja washiriki kutoka nchi 186 wanachama wa Umoja wa Mataifa ambapo walipitisha azimio la utekelezaji la Copenhagen la kuweka watu kuwa kitovu cha maendeleo.

Akizungumza kwenye mkutano wa leo, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Mogens Lykketoft amesema kumekuwepo na mafanikio katika kipindi cha miaka 15 tangu mkutano huo lakini ajenda 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu itachagiza kupatia suluhu mambo yanayokwamisha maendeleo ya binadamu hususan umaskini.

Wajumbe walipata fursa ya kuzungumza na kutoa tathmini ambapo mwakilishi wa kudumu wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Macharia Kamau akazungumzia mafaniko katika kukwamua watu wenye ulemavu..

(Sauti ya Balozi Kamau)

Mafanikio ni kama vile vile mfuko wa kuwapatia watu wenye ulemavu fedha na vifaa ili waanzishe biashara zao, pia tumeanzisha mfumo wa kuwapatia fedha kama njia ya hifadhi ya jamii kwa wale wasioweza kujihudumia wao na wategemezi wao. Hii imeenda sambamba na huduma bure ya bima ya afya kwa wale wote waliojisajili kuwa wanaishi na ulemavu.”