Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakazi wa nyanda za juu wakumbwa na njaa zaidi:FAO

Wakazi wa nyanda za juu wakumbwa na njaa zaidi:FAO

Katika kuangazia siku ya milima duniani hii leo, shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limesema ingawa kiwango cha njaa ulimwenguni kimeripotiwa kupungua, bado idadi ya wakazi wa milimani wasio na uhakika wa chakula imeongezeka kwa asilimia 30 kati ya mwaka 2000 na 2011.

Likinukuu utafiti mpya uliotolewa leo, FAO imesema wakazi wa nyanda za juu katika nchi zinazoendelea ndio waathirika zaidi ikisema mabadiliko ya tabianchi kwenye maeneo hayo yamezidi kuleta machungu, sambamba na hatari ya wakazi hao kukosa chakula.

Mkurugenzi Mkuu wa FAO Jose Graziano da Silva amesema wakati dunia inajielekeza kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu ni vyema jamii ya kimataifa kuwekeza maeneo ya milimani na kusaidia ubia wa shirika hilo na wadau wanaoendeleza nyanda za juu.

Utafiti huo umetaja vile ambavyo mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri wakazi hao na kusababisha njaa, mathalani ongezeko la kiwango cha joto kusababisha wadudu waharibifu na magonjwa kuweza kufika maeneo ya milimani.