Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zeid aonya dhidi ya hatari ya machafuko zaidi kuelekea uchaguzi CAR

Zeid aonya dhidi ya hatari ya machafuko zaidi kuelekea uchaguzi CAR

Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein, amelaani vikali machafuko ya kikabila yanayoendelea nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, na kuelezea hofu yake juu ya matumizi ya lugha za kidini akionya kwamba hii inaweza kuwa na madhara makubwa na kuleta hali tete kabla ya uchaguzi. Flora Nducha na taarifa Zaidi.

(TAARIFA YA FLORA NDUCHA)

Zeid amesema hali hiyo inaweza kuchochea wimbi lingine la mashambulizi nchini humo, pia akitiwa hofu na pande zote nchini humo ikiwemo serikali kwa kutoa wito wa kuanzishwa kwa makundi ya wanamgambo.

Amesema ongezeko la tabia miongoni mwa wakristo na waislamu kuunda makundi ya kujihami na kumtenga mtu yeyote asiyekuwa katika jamii yao kunatia wasiwasi na jamii mchanganyiko zinaweza kutoweka kabisa.

Ametoa wito kwa serikali kuchukua hatua haraka kudhibiti ghasia na chuki na kuhakikisha uwajibishwaji kwa ukiukwaji wa haki za binadamu.Pia ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa kuwataka wafuasi wao kushiriki kwa Amani katika kura ya amaoni ya katiba mwishoni mwa wiki na katika uchaguzi wa rais na wabunge utakaofanyika wiki mbili zijazo.