Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa OCHA kuzuru Syria Jumamosi Disemba 12

Mkuu wa OCHA kuzuru Syria Jumamosi Disemba 12

Mratibu Mkuu wa masuala ya kibinadamu, Stephen O’Brien atafanya ziara nchini Syria kuanzia kesho Jumamosi tarehe 12 hadi tarehe 14 Disemba 2015, ili kutathmini huduma za kibinadamu na kujionea athari za mapigano na operesheni za kijeshi dhidi ya raia.

Wakati mzozo wa Syria unapoingia majira ya baridi kali kwa mwaka wa tano, zaidi ya watu milioni 13.5 nchini humo wanahitaji usaidizi wa mahitaji ya msingi na ulinzi. Inakadiriwa kuwa familia nne kati ya tano nchini Syria zinaishi katika umaskini, huku mamilioni ya watu wakiwa hawana chakula cha kutosha, maji safi wala makazi.

Wakati wa ziara yake, Bwana O'Brien anatarajiwa kukutana na familia za watu waliofurushwa makwao, pamoja na maafisa wa ngazi ya juu na wadau wa mashirika ya kibinadamu, ili kujadili njia za kuimarisha jinsi ya kuwafikia raia kwa ajili ya kuokoa uhai wa watu wengi zaidi.